Subscribe For Free Updates!

We'll not spam mate! We promise.

Thursday 21 January 2016

SSRA yazindua mfumo wa kielektroniki kupokea malalamiko




Mkurugenzi wa Utafiti, Tathmini na Sera, Ansgar Mushi.Mkurugenzi wa Utafiti, Tathmini na Sera, Ansgar Mushi.

 MAMLAKA ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imeanzisha utaratibu mpya wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wanachama kwa kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Kwa watumiaji wa simu za mkononi, huduma hii hupatikana kwenye Google play kwa jina la SSRA. Mwenye malalamiko anaweza kutembelea tovuti ya www.ssra.go.tz na kutoa maoni kwenye sehemu iliyoandikwa malalamiko na maoni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo, Ansgar Mushi, Mkurugenzi wa Utafiti, Tathmini na Sera, amesema kuwa uanzishwaji wa mfumo huo ni moja ya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na SSRA katika kulinda na kutetea masilahi ya wanachama.
“Uanzishwaji wa mfumo huu ni moja ya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Mamlaka katika kulinda na kutetea masilahi ya wanachama kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Na. 8 ya mwaka 2008 iliyorekebishwa kwa sheria  Na. 5 ya mwaka 2012,” amesema Mushi.
Utaratibu huu wa kielektroniki umeanzishwa ili kumrahisishia mwanachama au mwananchi yeyote kutoa malalamiko  au maoni ya kuboresha sekta hii kwa maendeleo ya jamii  akiwa mahali popote kwa muda muda wowote kuhusu masuala ya sekta ya hifadhi ya jamii.
Mwanachama akishaingiza taarifa zake binafsi kama jina lake la kwanza, la kati na la ukoo, anuani ya posta, namba ya simu, namba ya uanachama na makazi ya mlalamikaji, mfumo hutoa namba ya kumbukumbu kwa mlalamikaji.
Taarifa binafsi za mlalamikaji husaidia kumtambua na kufanya mawasiliano na mwanachama mwenye tatizo. Kupitia Idara ya Utekelezaji na Uandikishaji mamlaka hupokea taarifa za wanachama na na malalamiko yaliyoingizwa kwenye mfumo kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa kufuatilia na kuwasiliana na mwanachama huyo kwa kupitia taarifa zake alizosajilia  kwenye mfumo wa kielektroniki.
“Kwa ujumla mawasiliano kati ya wananchi na Mamlaka yamerahisishwa kwa matumizi ya simu za mkononi kwa njia zilizoorodheshwa hapo juu. Pia Mamlaka ina utaratibu wa kuwasiliana na wadau kwa kutumia ujumbe ufupi (sms)  na barua pepe pamoja na namba ya simu ya 0762440706 ambayo inaingiza ujumbe wowote moja kwa moja kwenye mifumo ya kielektroniki,” ameongeza
Mushi amewataka wanachama kudumu kwenye mifuko yao ya kijamii hasa kipindi mwanachama anapoajiriwa na kampuni nyingine sababu kuna faida nyingi mwanachama akidumu kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii.
“Kuna faida mwanachama anapodumu kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii, mwanachama anapochangia kwenye mfuko hupata faida ya 2.7 ya mchango wake kwa mwaka. Anapodumu kwenye mfuko mmoja hadi kustaafu kwake ana uhakika wa kupata kiinua mgongo kinachoridhisha kuliko yule anayehama sababu anaanza moja,” amesema
Akijibu swali la mwandishi wa habari juu ya mwamko wa wananchi kujiunga na mifuko ya kijamii, amesema wananchi wengi wanakosa fursa ya kujiunga mifuko ya hifadhi ya jamii kutokana na sheria zilizowekwa kubana wananchi ambao hawajaajiriwa, ingawa hivi karibuni mifuko ya kijamii imejitahidi kulegeza sheria na kuruhusu wasioajiriwa kujiunga na mifuko ya hiyo.
Mushi amewataka wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na umma kutumia huduma hii kwani ni rahisi kutumia, ina uwazi na haihitaji mwanachama  au mdau kufika katika ofisi za mamlaka; inaokoa muda, nauli na kuboresha huduma kwa wanachama.

Na Regina Mkonde